Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, ameseme Serikali ya Awamu ya Sita itaimarisha zaidi sekta ya Nishati ili kuhakikisha Nchi inazalisha umeme wakutosha.

Mhe. Mpango ameyasema hayo jana Julai 15, 2021, wakati akiweka jiwe la msigi la ujenzi wa mradi wa kusafirisha Umeme wa Kilovoti 132, kutoka Tabora hadi Kigoma pamoja na kituo cha kupoza Umeme Nguruka mkoani Kigoma.

Mradi huu unalenga kuboresha upatikanaji wa umeme Kaskazini Magharibi mwa Tanzania na kuunganisha Mkoa wa Kigoma katika gridi ya Taifa.

“Tunahitaji umeme wa uhakika ili tuweze kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo na kukidhi mahitaji muhimu ya kiuchumi kwa ajili ya matumizi ya majumbani, lakini pia matumizi ya Viwanda” amesema Mhe. Mpango

“Uzuri sehemu kubwa ya mradi huu mnafanya wenyewe TANESCO, hivyo muhakikishe mnaharakisha, na ukamilike mwakani badala ya 2023” aliiagiza TANESCO Mhe. Mpango

Aidha, Mhe. Mpango amesema ni muhimu sasa ajenda ya kuufungua zaidi Mkoa wa Kigoma itekelezwe kwa kasi, kwa kuboresha miundombinu yote ikiwemo ya umeme.

Naye Naibu Waziri wa Nishati, Wakiki Mhe. Stephen Byabato amesema kituo cha Nguruka kitakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 36, na njia ya kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi Kigoma itaimarisha upatikanaji wa umeme Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.

“Njia yote ina taklibani kilometa 393, itajengwa na TANESCO pamoja vituo vya kupoza umeme vya Uhuru – Urambo na Nguruka – Uvinza, vitajengwa na TANESCO wenyewe” amesema Naibu Waziri

Aidha, Mhe. Byabato amesema katika jitihada mbadala za kuboresha upatikanaji umeme katika Mkoa wa Kigoma, wakati ukisubiriwa mradi ukamilike, TANESCO itapeleka mashine moja kutoka Loliondo ambako tayari grid ya Taifa imefika, ili iweze kuboresha upatikanaji wa umeme Wilaya Kasulu – Kigoma.

Jumla ya gharama za mradi huu kwa awamu ya kwanza ni Shilingi bilioni 66.7. Kati ya kiasi hicho gharama za vituo vya kupoza umeme kwa awamu ya kwanza ni Shilingi bilioni 6.8 kwa kituo cha Uhuru na Shilingi bilioni 6.2 kwa kituo cha kupoza umeme cha Nguruka.