Makundi kadhaa yanayoiunga mkono Iran nchini Iraq yamepongeza tamko la Marekani kwamba inapanga kuyaondoa rasmi majeshi yake yanayopigana nchini Iraq hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Makundi hayo yamesema yamekuwa yakiitaka Marekani ichukue hatua kwa muda mrefu. Marekani imesema badala yake itatoa mafunzo na ushauri tu kwa majeshi ya Iraq.
Taarifa hiyo imetolewa baada ya rais Joe Biden kukutana na waziri mkuu wa Iraq Mustafa al-Kadhimi kwenye ikulu ya Marekani. Wanajeshi wapatao 2,500 wapo nchini Iraq kwa sasa, wanasaidia kupambana na wapiganaji wa kundi linalojiita dola la kiislamu IS.
Wakati huo huo Marekani imeahidi kuipa Iraq takriban dozi laki 5 za chanjo dhidi ya COVID-19.
Biden amesisitiza msaada wa Marekani katika uchaguzi wa nchini Iraq utakaofanyika mwezi Oktoba, amesema Marekani inashirikiana kwa karibu na Iraq, Baraza la Ushirikiano la Ghuba na Umoja wa Mataifa kuhakikisha uchaguzi huo utakuwa wa haki.