Umoja wa Ulaya umependekeza marufuku ya uuzaji wa magari yanayotumia petroli na dizeli itakapofikia mwaka 2035. Pendekezo hili ni sehemu ya pendekezo kubwa la kimazingira litakaloharakisha kugeukia matumizi ya magari yanayotumia umeme ambayo hayatoi gesi ya aina yoyote. 

Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya imependekeza kwamba ifikiapo mwaka 2030 gesi chafu ya kaboni inayotolewa na magari itapunguzwa kwa asilimia 55, lengo hilo likiwa juu zaidi ya lile lililopo sasa la kupunguza gesi hiyo kwa asilimia 37.5 ifikiapo mwaka huo. 

Halmashauri hiyo pia imesema ifikiapo mwaka 2035 magari yanayotumia petroli na dizeli hayatouzwa tena katika nchi za Umoja wa Ulaya hivyo gesi chafu ya kaboni kutoka kwenye magari itakuwa imeondolewa hewani kwa asilimia mia 100.