Mafuriko mengine yameyakumba baadhi ya maeneo nchini Ubelgiji na kusomba magari baada ya mvua kubwa iliyoambatana na ngurumo za radi kunyesha nchini humo hapo jana Jumamosi. 

Majimbo ya Namur na Walloon Brabant Kusini Mashariki mwa mji mkuu Brussels yameathirika zaidi kutokana na mvua hiyo. Maeneo hayo pia yaliathirika wakati wa mafuriko ya wiki iliyopita yaliyosababisha vifo vya watu 36 na kupotea kwa wengine saba. 

Kituo cha kushughulikia majanga nchini Ubelgiji, kilikuwa kimetoa tahadhari kwa watu nchini humo huku hali mbaya ya hewa ikitarajiwa kudumu kwa siku kadhaa. 

Wataalam wanasema kuwa mafuriko kama haya yatatokea mara kwa mara na kuwa mabaya zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi huku mataifa yakihitajika kubadilika katika hatua zinazojumuisha kufanya tathmini mpya kuhusu athari za mafuriko ya siku zijazo , kuimarisha mifumo ya tahadhari na kuwaandaa watu kuhusu majanga sawa na hayo.