Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kaskazini ya KCMC iliyopo mkoani Kilimajaro, imepokea mitungi 300 ya Oksijeni kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wenye changamoto ya upumuaji waliolazwa katika hospitali hiyo.

Mitungi hiyo ya Oksijeni imetolewa na Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD), siku chache baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC, Profesa Gilleard Masenga kueleza kuwa wamezidiwa na Wagonjwa wanaohitaji hewa hiyo ya Oksijeni kupumua.

Profesa Masenga amesema hospitali hiyo ya KCMC yenye kinu cha kuzalisha Oksijeni kikiwa na uwezo wa kujaza mitungi 400 kwa siku, kimezidiwa kutokana na ongezeko la wagonjwa ambapo mgonjwa mmoja amekuwa akitumia mitungi 10 kwa siku.

Kabla ugonjwa wa corona kuingia nchini, hospitali hiyo ya Rufaa Kanda ya Kaskazini ilikuwa ikitumia kati ya mitungi 50 na 60 kwa siku lakini sasa inatumia mitungi zaidi ya 400.