Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM,) Daniel Chongolo amemwagiza mkuu wa mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti kuunda kikosi kazi cha kukagua na kufanya tathmini ya miradi inayotekelezwa mkoani humo ili kujua ikiwa utekelezaji wake unakidhi thamani ya fedha zilizotumika.

Pia  amesema  hakuridhishwa na miradi walioitembelea hasa katika  sekta ya afya ambayo  inayokabiliwa na changamoto kubwa ya dawa, wataalam, huduma duni kwa wazee pamoja na  maeneo mengine kuwa na  utekelezaji wa miradi isiyoendana na thamani ya fedha iliyotumika.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa chama hicho,Daniel Chongolo katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku mbili mkoani humo aliyoambatana na wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa kilichofanyika ukumbi wa mikutano manispaa ya Sumbawanga.

"Naagiza na kukuelekeza  mkuu wa mkoa  uunde timu ya wataalam kwa ajili ya kukagua na kufanya tathmini ya miradi yote inayotekelezwa mkoani kwako ili kujua hali halisi ya kinachoendelea hususani kwenye eneo la thamani ya fedha zilizotumika hapa mambo hayaendi vizuri kabisa" Alisema  Chongolo.

Alisema  kuwa CCM haiko tayari kuwalea viongozi na watendaji wazembe wanaoonekana kushindwa kutatua kero za wananchi na kuimarisha ustawi wao hivyo kati siku 14 atahitaji kupata ripoti ya utekelezaji wa maelekezo hayo na hatua kali zichukuliwe itakapobainika kuna ubadhirifu ama uzembe ambao unakwambisha ufanisi wa miradi hiyo.

Hata hivyo Chongolo alisema atakaporejea Dodoma watawaita mawaziri wanaohusika na sekta za afya maji, aridhi na tamisemi ili kujiridhisha juu ya mipango yao na kujua mkwamo ama urasimu unatokea katika eneo gani na kupelekea huduma kusuasua na kuwa sio za kiwango na ufanisi kwa wananchi.