Mahakama ya Wilaya ya Serengeti imemhukumu kifungo cha miaka 60 jela Adamu Matera (22) mkazi wa kijiji cha Remung’orori kwa kosa la kumbaka na kumpa mimba mwanafunzi wa darasa la sita.

Katika hukumu iliyosomwa na Hakimu mkazi wa wilaya, Judith Semkiwa mshtakiwa ametiwa hatiani kwa makosa mawili la kubaka na kumpa mimba mwanafunzi huyo kinyume cha sheria.

Katika kosa la kwanza la ubakaji, Matera amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kosa la pili la kumpa mwanafunzi mimba nalo akihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.

Hata hivyo adhabu zote zinakwenda pamoja hivyo mshtakiwa huyo atatumikia kifungo cha miaka 30 gerezani.

Mwendesha Mashtaka wa Jamhuri, Faru Mayengela akiieleza mahakama katika kesi ya Jinai namba 264/2020 mbele ya Hakimu Semkiwa amesema mshtakiwa alitenda kosa hilo kati ya Machi na Mei 2020.

Amesema mshtakiwa mwenye wake wawili alianza mahusiano ya kimapenzi na mtoto mwanafunzi huyo kisha akampa mimba na kufikishwa mahakamani hapo kwa makosa mawili la kubaka na kumpa mimba mwanafunzi.