Vyombo vya usalama nchini Afrika Kusini vimethibitisha kwamba aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma amejisalimisha mwenyewe polisi, ikiwa imepita wiki moja tangu alipopatikana na hatia ya kuidharau Mahakama kufuatia kesi yake ya ufisadi na kuhukumiwa kifungo cha miezi 15 gerezani.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, usiku wa kuamkia leo umekuwa ni wa kwanza gerezani kwa Jacob Zuma, baada ya kujisalimisha mwenyewe kwa mamlaka husika jana usiku.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, Rais huyo mstaafu ameamua kutii agizo la kufungwa kwake.

Baada ya kufikia makubaliano ya kujisalimisha kwake na ujumbe wa polisi uliofika nyumbani kwake mapema jana, Rais mstaafu wa Afrika kusini Jacob Zuma, akisindikizwa na walinzi wake alienda katika gereza lililo karibu na nyumbani kwake katika jimbo la KwaZulu Natal.

Baadhi ya wafuasi wake waliokuwa wamekusanyika nje ya nyumba yake walionyesha kutofurahishwa kuhukumiwa kifungo gerezani kiongozi wao huyo.