Idadi ya waliokufa kutokana na moto mbaya uliolipuka kusini mwa Iraq katika wodi ya hospitali inayotumiwa na wagonjwa wa COVID-19 imeongezeka na kufika watu 58 huku vyombo vingine vya habari vikitaja kuwa imefika 64. 

Maafisa wawili wa afya wamesema watu wengine wapatao 100 wamejeruhiwa katika moto huo wa hospitali ya Imam al-Hussein kwenye mji wa Nassiriya nchini Iraq. 

Aidha wameongeza kuwa moto huo uliotokea jana usiku umesababishwa na kuripuka kwa mtungi wa gesi. 

Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al-Kadhimi amefanya mkutano wa dharura wa mawaziri na makamanda wakuu wa usalama kujadiliana kuhusu mkasa huo. 

Mfumo wa afya wa Iraq ulioharibiwa kwa vita na vikwazo, umekuwa ukipambana kukabiliana na janga la virusi vya corona ambalo limewaua watu wapatao17,592 na wengine zaidi ya milioni 1.4 wakiwa wameambukizwa.