Zaidi ya watu 120 wamekufa kufuatia mafuriko makubwa katika maeneo ya magharibi mwa Ujerumani na Ubelgiji. Operesheni zinaendelea za kuwatafuta na kuwaokoa mamia ya watu ambao bado hawajulikani waliko au wako hatarini. 

Maafisa katika jimbo la Ujerumani la Rhineland-Palatinate wamesema watu 60 wamefariki dunia, wakiwemo watu 12 katika makazi ya watu wanaoishi na ulemavu katika mji wa Sinzig. 

Katika jimbo jirani la North Rhine-Westphalia maafisa wamesema idadi ya vifo ni 43 lakini wameonya kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka. 

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema ameshtushwa na uharibifu uliosababishwa na mafuriko na akaahidi kuzisaidia familia za waliopoteza maisha na miji na vijiji vinavyokumbwa na uharibifu. 

Katika nchi jirani Ubelgiji, maafisa wamethibitisha kuwa watu 18 wamekufa na 19 hawajulikani waliko.