Na Eliafile Solla-WANMM MTWARA
Dkt. Angeline Mabula Naibu Waziri Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema amesikitishwa na wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi mkoani Mtwara kutokana na uzito wao katika kutii sheria, kanuni, taratibu na masharti ya umiliki ardhi ambayo sharti mojawapo ni kulipa kodi hiyo kila mwaka.

Hayo yalijitokeza wakati Dkt. Angeline Mabula alipokuwa akizungumza na wadaiwa hao wa kodi ya pango la ardhi katika kikao maalum kilichohusisha watendaji wa sekta ya ardhi mkoani Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mikindani, Bw. Dustan Kyobya, Mkurugenzi wa Halmashauri kanal Emanuel Mwaigobeko pamoja na mbunge wa jimbo la Mtwara mjini Mhe. Hassan Mtenga.

‘‘Wanamtwara mmekuwa wazito na wagumu sana katika ulipaji wa kodi ya pango la ardhi licha ya jitihada za kuwakumbusha mara kwa mara pamoja na kuwaletea ankara za madai, bado hamuonyeshi ushirikiano, mnaahidi lakini hamtekelezi na hivyo tutaruhusu sheria kuchukua mkondo wake japo siyo lengo la Serikali, alisema Dkt. Angeline Mabula’’

Aidha, katika kusisitiza kuhusu umuhimu wa kodi ya pango la ardhi, Dkt. Angeline Mabula alisema taifa la Tanzania linajengwa na watanzia wenyewe kupitia kodi mbalimbali wanazolipa ikiwemo kodi ya pango la ardhi ambayo mwisho hurudishwa kwao kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo.

‘‘Katika ujenzi wa taifa, Serikali inawategemea wananchi na wananchi wanaitegemea Serikali hivyo maendeleo ya nchi ni ushirikiano wetu wananchi na Serikali kwa maana hiyo kodi ya pango la ardhi ina mchango mkubwa sana katika ukuaji wa uchumi, alisema Dkt. Mabula’’

Katika hatua nyingine, Dkt. Angeline mabula alidokeza kwamba, Serikali ilikusudia kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia vipande vya ardhi wanavyomiliki na hivyo kuanzisha mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha kila kipande cha ardhi kwa lengo la kuiongezea thamani ardhi na kuwanufaisha wamiliki.

‘‘Pamoja na jitihada hizi za Serikali bado wanamtwara mmekuwa wakaidi, hamtaki kuchangia hata zile gharama ndogo za upimaji na mliopimiwa hamuoni haja ya kumilikishwa na kuchukua hati zenu mkazitumie kama vyanzo vya mitaji ili kujiendeleza kiuchumi, alisema Dkt. Mabula’’

Nae mbunge wa Mtwara mjini Mhe. Hassan Mtenga aliwaambia wadaiwa hao kwamba, suala la kodi ya pango la ardhi siyo la hiari, ni sharti la kisheria na ni kodi rafiki endapo italipwa kwa wakati bila kusubiria hadi ijilimbikize na endapo haitalipwa sheria iko wazi imebainisha hatua zitakazochukuliwa kwa watakaokaidi.