Rais Wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  amesema umefika wakati wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuunda tume ya kupambana na Udhalilishaji wa Kijinsia visiwani Zanzibar kwa ajili ya kupambana na udhalilishaji visiwani humo. 


Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo kwenye  kongamano la udhalilishaji liloandaliwa na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake wa Zanzibar katika ukumbi wa Shekh Idriss Abdul - Wakil, Kikwajuni Jijini Zanzibar.


 Aidha Mhe. Rais Mwinyi amewataka watendaji wa Taasisi zote zinazohusika na suala la udhalilishaji kujipima juu ya utendaji wao. Hii ni baada ya kuendelea kutolewa malalamiko Kwa baadhi ya watu ambao wanashutumiwa Kwa vitendo vya udhalilishaji kuachiliwa huru.


Udhalilishaji sio suala la ubakaji tu, kwani waathirika wakubwa japo wanaonekana ni wanawake lakini wapo wanaume wengi ambao wanadhalilishwa pia. Alisema Mhe. Rais Mwinyi.


“Nimekuja hapa kuwapeni Uhakika wa kwamba ninayo dhamira ya dhati kulimaliza tatizo la udhalilishaji visiwani kwetu. “


Katika hatua nyingine, Mhe. Rais amemtaka Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Omary Makungu kuwahimiza majaji na mahakimu waliochini ya Mhimili wake kutekeleza wajibu wao Kwa wakati na Kwa Uadilifu ili kulinda haki za watu ambao wametendewa unyanyasaji wa kijinsia.


Mhe.  Rais, Dk. Mwinyi, amezishukuru taasisi na asasi binafsi ambazo zimekuwa zikitoa misaada ya kisheria kwa Wananchi wa Zanzibar kwani licha ya Kwamba ni wajibu wa Serikali kutoa huduma na misaada ya kisheria, lakini taasisi hizi zimekuwa msaada mkubwa.