Jeshi la Polisi wilayani Geita linamshikilia Vicent Said (27) mkazi wa Kata ya Magenge kwa tuhuma za kumbaka mwanaye wa kambo mwenye umri wa miaka saba.

Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Henry Mwaibambe, wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema, tukio hilo limetokea Julai 2, mwaka huu katika kijiji cha sobora ambapo mtuhumiwa huyo anadaiwa kumrubuni mtoto huyo kwa maandazi na juisi ya shilingi 500.

Kamanda Mwaibambe amesema mtuhumiwa amekamatwa na atafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.

Aidha, Kamanda huyo amesema baada ya tukio hilo kuna watu wanaotaka kuharibu ushahidi ili mtuhumiwa aachiwe huru na kuwatahadharisha kuziacha juhudi hizo mara moja kwani polisi hawatozifumbia macho ili haki itendeke.

Akizungumza na chombo kimoja cha habari, mtoto huyo aliyefanyiwa kitendo hicho, amesema baba yake huyo amekuwa akimfanyia kitendo hicho mara kwa mara na pindi anapomfanyia humfunga mdomo na akimaliza humnunulia maandazi na juisi.