Happy Lazaro, Arusha.
Arusha.Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha,linamshikilia Melita Ndaletyan(34) kwa tuhuma za kumuua kaka yake Kiseri NdaIetyan ( 38),baada ya marehemu  kumzuia mtuhumiwa aliyekuwa akitaka kumwingilia kimwili mke wa kaka yao mkubwa.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha leo,Justine Maseju,alisema tukio hilo lilitokea Julai 8 2021 majira ya saa 6:30 usiku,katika Kitongoji cha Naamalasin,Kata ya Noondoto wilayani Longido mkoa wa Arusha.


Alidai  kuwa Kiseri alifariki dunia baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni na mdogo wake ambapo wote wawili ni wafugaji ambapo ndugu wote watatu wanaishi kwsnyw boma moja na kuwa siku ya tukio mtuhumiwa alitaka kutenda kosa hilo kwa mke wa kaka yake ambaye hakuwepo nyumbani wakati huo.


Kamanda amesema kwa mujibu wa uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni tamaa ya kimapenzi ambapo mtuhumiwa huyo anadaiwa kutaka kumwingilia kimwili mke wa kaka yake na kuzuiwa na marehemu kufanya jambo hilo jambo lililosababisha ugomvi kati yao.


“Mtuhumiwa,marehemu pamoja na kaka yao mwingine wote walikuwa wanaishi kwenye boma moja hivyo mtuhumiwa wakati anataka kumwingilia kimwili mke wa kaka yake(mkubwa) ambaye hakuwepo nyumbani,marehemu alitokea na kumkataza kufanya hivyo ndipo mtuhumiwa alimchoma na kitu chenye ncha kali,”


“Jeshi la Polisi linaendelea kumshikilia mtuhumiwa kwa kumfanyia ukatili ndugu yake na mara baada ya upelelezi kukamilika jalada litapelekwa Ofisi ya mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria,”


Kwa mujibu wa Kamanda mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa familia kwa ajili ya taratibu za maziko baada ya mwili huo kufanyiwa uchunguzi