Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema serikali yake ya shirikisho itashirikiana na majimbo ya Magharibi mwa Ujerumani yaliyoathirika kwa mafuriko kuzijenga upya jamii. 

Akizungumza baada ya kuwasili mjini Schuld, moja ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko, Merkel ameielezea hali katika maeneo hayo kuwa ya kutisha. 

Merkel ambaye ameahidi msaada wa haraka wa kifedha, pia amezipongeza juhudi za uokozi zinazoendelea na mshikamano aliyouona wakati wa ziara hiyo, lakini ameonya kwamba shida kwenye eneo hilo hazitotatuliwa haraka. 

Amesema kinachohitajika sasa ni sera inayozingatia maumbile na mabadiliko ya tabianchi kuliko ilivyofanyika katika miaka ya hivi karibuni. Maafa hayo yamesababisha vifo vya watu 110 katika wilaya ya Ahrweiler iliyoko kwenye jimbo hilo. 

Watu wengine 670 wamejeruhiwa. Vifo vingine 46 vimeripotiwa katika jimbo jirani la North-Rhine Westphalia.