Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuna viashiria vya kutokea kwa wimbi la tatu la mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 nchini, hivyo imewakumbusha na kuwatahadharisha wananchi kuchukua tahadhari.

Tahadhari hiyo imetokana na hali ya mwenendo wa ugonjwa huo duniani na ongezeko la maambukizi katika nchi za Afrika ambapo maambukizi yameendelea kuongezeka maradufu kuliko ilivyokuwa katika wimbi la pili.

“Jukumu la kinga dhidi ya ugonjwa huu ni la kila mmoja wetu, hivyo tusiwe na hofu ila tuendelee kuzingatia afua za kinga,” imeeleza taarifa ya wizara.

Kutokana na tishio hilo, wizara imewataka wananchi kuendelea na utamaduni wa kunawa mikono kwa sabuni, uvaaji wa barakoa ambazo mhusika ametengeneza mwenyewe au zimetengenezwa nchini, kufanya mazoezi, kupata lishe bora, kuepuka misongamano na kuwahi vituo vya afya.

Wizara imewakumbusha wananchi kuendelea kutoa taarifa zozote za kiafya na kupata ufafanuzi wa masuala ya kiafya kupitia namba ya simu 199 bila malipo yoyote na kufuatilia na kuzingatia taarifa za mwenendo wa ugonjwa huu kutoka vyanzo rasmi vya serikali.