Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb.) amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Marekani hapa nchini Mhe. Dkt. Donald J. Wright, jijini Dodoma jana  tarehe 15 Juni 2021.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano baina nchi hizi mbili.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Balozi Mulamula amemhakikishia Balozi Wright ushirikiano hususan kupitia Sekta muhimu ambazo nchi hizi mbili zinashirikiana kwa muda mrefu ikiwemo sekta ya afya, elimu, miundombinu, teknolojia, uwekezaji na biashara.

"Leo nimekutana na Balozi wa Marekani hapa nchini ikiwa ni utaratibu niliojiwekea wa kukutana na Mabalozi wawanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania mara kwa mara kwa  lengo la kubadilishana nao mawazo kuhusu namna bora ya kuimarisha uhusiano wetu na nchi hizo. Katika mazungumzo yangu na Balozi Wright tumejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo mpango wanaoufadhili wa kupambana na UKIMWI wa PEPFAR na jambo kubwa amenijulisha kuwa Marekani ipo tayari kushirikiana na Tanzania na kwamba kampuni nyingi za nchi hiyo zipo tayari kuja kuwekeza na kufanya biashara hapa nchini wakati wowote kuanzia sasa” alisema Balozi Mulamula.

“Pia amenifahamisha kuwa, Tanzania mwaka huu imekuwa miongoni mwa nchi za Afrika zinazostahili kupeleka bidhaa zake za kilimo nchini Marekani bila kutozwa ushuru kupitia Mpango wa AGOA. Hii ni fursa muhimu kwetu na kinachotakiwa sasa ni sisi kujiimarisha katika kuzalisha bidhaa bora zitakazokidhi vigezo vya kuingia kwenye soko la Marekani” alisisitiza  Mhe. Waziri.

Kwa upande wake, Balozi Wright amemshukuru Mhe. Balozi Mulamula kwa kumpokea na kueleza kuwa nchi yake inathamini na kuuenzi ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati yake na Tanzania na kwamba itaendelea kuuimarisha ushirikiano huo kwa kuchangia sekta mbalimbali.

“Nimekuwa na mkutano mzuri na Mhe. Balozi Mulamula na tumejadili masuala muhimu na yenye manufaa kwa nchi zetu mbili hususan umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kupitia sekta mbalimbali. Marekani inaihesabu Tanzania kama rafiki na mshirika muhimu hivyo mkutano huu ni moja ya jitihada za kuimarisha ushirikiano na urafiki huo” alieleza Balozi Wright.