WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara, Taasisi, Mashirika yote ya Serikali na Sekta Binafsi pamoja na vikundi vya uzalishaji zinazotumia nishati ya kuni na mkaa zianze kutumia nishati mbadala kwa  kupikia na shughuli nyingine za uzalishaji.

Ametoa wito huo leo (Jumanne Juni Mosi, 2021) wakati akitoa tamko kuhusu Wiki ya Mazingira Duniani, katika ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma.

Amesema kuwa taasisi kama shule, vyuo, hospitali na majengo makubwa  zinapaswa kuzingatia ufungaji wa mifumo ya nishati ya gesi kwa ajili ya kupikia.

“Kila Wizara ifanye ufuatiliaji kwenye taasisi zake na nipatiwe taarifa ya hali ya utekelezaji kila baada ya miezi sita inayoonesha ni taasisi ngapi zimefikiwa, zimebadili mifumo au zimejenga majengo kwa kuzingatia hitaji la nishati mbadala”

“Suala la uhifadhi, utunzaji, usimamizi na usafi wa mazingira lisiwe jambo linalofanyika wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani pekee, bali tujenge tabia ya kuliona kwamba ni suala la kila siku” amesisitiza

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa Jiji la Dodoma wahakikishe wanaweka mkakati ili maeneo yote yanayopimwa yapandwe miti na kila anayepata kiwanja aelimishwe kuhusu umuhimu wa kupanda miti.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo amesema kuwa katika maadhimisho haya watafanya semina  kwa maafisa mazingira kutoka TAMISEMI. “Maafisa mazingira hawa hawakuwa wanatumika vizuri, kupitia maadhimisho haya tutabadilishana mawazo  na kujua nini cha kwenda kufanya kuhusu agenda ya mazingira”.

Amesema kuwa kutakuwa na kampeni kabambe itakayohusisha wadau mbalimbali wa maendeleo lengo likiwa ni kuhakikisha Tanzania inakuwa  nchi ya mfano duniani katika utunzaji mazingira "kampeni hii itakuwa endelevu, afua mbalimbali za mazingira zitaongeza thamani katika kampeni hiyo"

MWISHO.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,