WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekabidhi magari ya wagonjwa 20 yenye thamani ya sh. bilioni 2.24 ambayo yatapelekwa kwenye vituo vya afya 13, hospitali za halmashauri tano, ya wilaya moja na ya rufaa ya mkoa moja katika mikoa 17.

Akikabidhi magari hayo jana (Jumanne, Juni mosi, 2021) katika hafla fupi iliyofanyika ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma, Waziri Mkuu amezitaka Halmashauri zitenge fedha za matengenezo (motor vehicle services) ili kuhakikisha magari hayo yanadumu kwa muda mrefu zaidi.

“Iko tabia katika baadhi ya Halmashauri kutosimamia haya magari kwa maana ya kutotenga fedha za kuyafanyia service kila inapotakiwa. Lazima gari lihudumiwe ili litumike kwa muda mrefu zaidi,” amesema.

Amewaomba Wabunge waliopokea magari hayo wakayasimamie ili yatoe huduma inayotarajiwa kwa wananchi. “Msisite kuyaeleza haya masuala kwenye mabaraza ya madiwani ili wahusika wazingatie jukumu la kuyatunza,” amesisitiza.

Amesema mwaka jana alikabidhi magari 50 ya kubebea wagonjwa kati ya 70 yaliyokuwa yamepangwa kutolewa ili kuboresha huduma za afya nchini.

“Mhehishimwa Rais Samia ameridhia magari haya yatolewe na yaende yakatoe huduma kwa wananchi. Pia ameridhia hospitali za mikoa na wilaya ziwe na magari ya kubeba wagonjwa na kuwaleta kwenye huduma kwa haraka.”

“Magari haya ni mazuri na yana uwezo wa kwenda kilometa zaidi ya 500 hadi 1,000 kwa hiyo mgonjwa anaweza kutolewa Mbeya na kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili au akaletwa Hospitali ya Benjamin Mkapa hapa Dodoma bila shida yoyote,” ameongeza.

Ameishukuru taasisi ya Global Fund (Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria) kwa kuwezesha ununuzi wa magari hayo mapya kupitia Mradi wa Kuimarisha Mifumo ya Afya iliyo Thabithi na Endelevu (Resilient and Sustainable Systems for Health - RSSH Grant).

“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi thabiti wa Mama yetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu ninatoa shukrani za dhati kwa ufadhili huu wa magari haya ambayo yatatumika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Amesema upatikanaji wa magari hayo ni utekelezaji wa ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu na kwamba yakipatikana magari mengine bado yataendelea kutolewa ili kuimarisha utoaji wa huduma za tiba kwa wananchi.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na Wabunge waliofika kupokea magari hayo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Dorothy Gwajima alisema magari hayo 20, yatapelekwa kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga, hospitali ya wilaya ya Masasi, hospitali za halmashauri tano na kwenye vituo vya afya 13.

Alisema magari mitano yamepelekwa kwenye hospitali za Halmashauri za Mkalama (Singida), Ngorongoro (Arusha), Chunya (Mbeya), Buhigwe (Kigoma) na Nyamwaga iliyoko Tarime mkoani Mara.

Amevitaja vituo vya afya 13 vilivyopatiwa magari ni cha Kifanya (Njombe Mjini), Bwina (Chato), Iyula (Mbozi), Lubanda (Ileje), Kibaoni (Kilombero), Nakapanya (Tunduru Kaskazini), Kilongwe (Mafia) na Bwisya (Ukerewe). Vingine ni Kibutuka (Liwale), Nalasi (Tunduru Kusini), Mlete (Songea Mjini), Kambi ya Simba (Karatu) na Mnazi (Lushoto).

Akitoa shukrani kwa niaba ya Wabunge wenzake waliopokea magari leo, Mbunge wa Njombe Mjini, Bw. Deaodatus Mwanyika alisema wanashukuru kupokea magari hayo ambayo yametolewa ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Wakati wa kampeni, wewe, Mheshimiwa Rais wa awamu ya sita na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano mlipita kunadi sera na kuahidi wananchi mambo mbalimbali. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa utekelezaji wa haraka wa ahadi hizi,” alisema.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU