Waziri Lukuvi Aomba Undp Kusaidia Sekta Ya Ardhi Nchini
Na Munir Shemweta
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameliomba Shirika la Maendekeo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kusaidia juhudi za wizara ya ardhi katika kuendeleza sekta ya ardhi nchini.
Lukuvi aliwasilisha ombi hilo jana tarehe 17 Juni 2021 wakati wa mazungumzo yake na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la UNDP nchini Tanzania Christine Musisi yaliyofanyika ofisi za Wizara katika Mji wa Serikali eneo la Mtumba jijini Dodoma.
‘Ili kuiwezesha Wizara ya Ardhi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ni vyema tukawa na ushirikiano thabiti na UNDP kusaidia juhudi za wizara zenye lengo la kuleta matokeo chanya kwenye maendeleo ya ardhi’’ alisema Lukuvi.
Waziri Lukuvi alisema, ushirikiano kati ya Wizara ya Ardhi na UNDP utaisadia Tanzania kufikia malengo namba 11 yatakayoifanya miji yake kuwa salama kufikia mwaka 2030.
Kwa mujibu wa Lukuvi, hivi sasa wizara ya ardhi inatekeleza mpango wake wa miaka 10 wenye lengo la kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi na hivyo kuboresha usalama wa miliki za ardhi kwa watanzania.
Aidha, ameliomba Shirika la UNDP kuangalia uwezekano wa kuisadia wizara yake vifaa vya upimaji na magari kwa lengo la kurahisisha kazi za upimaji kwenye maeneo mbalimbali jambo alilolieleza kuwa litaisadia pia kutatua migogoro ya ardhi.
Mbali na mambo mengine, Waziri wa Ardhi alimueleza Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania kuwa, utekelezeji Mpango Kabambe nchini Tanzania bado una changamoto kwenye mamlaka za upangaji suala alilolieleza linasababisha maandalizi ya Mipango Kabambe kwenye mamlaka ya serikali za mitaa kutoenda kwa kasi kutokana na ukosefu wa fedha pamoja na wataalamu wa kutosha.
‘’ Kwa sasa Wizara imeidhinisha jumla ya mipango kabambe 26 katika miji sita, manispaa 13 pamoja na halmashauri za miji saba’’ alisema Lukuvi
Kuhusiana na Kongamano la Kitaifa la Miji, alisema kongamano hilo ni muhimu kwa kuwa linajumuisha mijadala inayohusu masuala ya sera kuhusiana na maendeleo endelevu ya miji katika ngazi ya kitaifa hasa kwenye utekelezaji agenda mpya ya miji na malengo ya maendeleo endelevu.
Mwakilishi mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP Chritistine Musisi alisema Shirika lake litaangalia namna ya kuisaidia wizara ya ardhi katika masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya ardhi nchini ili kuifanya sekta hiyo iweze kupiga hatua.
Bi. Musisi aliyeambatana na ujumbe wake katika ziara yake alisema, timu yake itakaa na timu ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuangalia maeneo yote ambayo Shirika lake linaweza kusaidia ikiwemo kongamano la kitaifa kuhusiana na masuala ya miji.
Waziri Lukuvi pia alianisha jitihada za wizara ya ardhi katika kuleta maendeleo ya sekta ya ardhi na kueleza kuwa pamoja na wizara hiyo kuanzisaha ofisi za ardhi za mikoa kwenye mikoa 26 ya Tanzania Bara pia inafanya maboresha kwenye mifumo yake ya utunzaji hati za ardhi kutoka analogia kwenda digitali sambamba na kuanzisha kituo cha Huduma kwa Wateja ambacho wananchi wataweza kuwasilisha kero za ardhi moja kwa moja kupitia njia ya simu.