Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amefuta waraka namba moja  unaowaondoa madiwani kushiriki katika shughuli za uidhinishaji mipango ya uendelezaji miji katika maeneo yao uliotolewa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi nchini.


Kabla ya kutolewa waraka huo mpya  Madiwani kupitia kamati zao za mipango miji walikuwa ndiyo wenye  mamlaka ya kubariki mipango ya uendelezaji miji katika halmashauri husika kupitia vikao vyao vya robo mwaka na waraka mpya unataka shughuli hizo sasa kufanywa na wataalamu wa mipango miji kwa kushirikisha sekta mbalimbali kama vile sekta za maji, barabara, umeme nk.

Lukuvi alifanya maamuzi hayo katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Meru wakati akizingumza na madiwani wa halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kusikiliza na kutatua kero za ardhi katika mkoa wa Arusha.

Alisema, kwa sasa waraka huo ameufuta mpaka utakapotolewa mwingine wenye maelekezo yatakayokuwa na tija na kusisitiza kuwa haiwezekani kuwaondoa madiwani kupitisha mipango ya uendelezaji miji katika  halmashauri zake kwa kuwa mamlaka ya upangaji bado ziko chini halmashauri.

" Nimeamua kuufuta waraka namba moja unaokataza madiwani kupanga mipango ya uendelezaji miji  katika halmashauri zenu, huwezi kuwa na halmashauri inayoshindwa kupitisha au kubariki mipango ya wilaya katika matumizi ya ardhi" alisema Lukuvi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, wataalam wa mipango miji katika ofisi za ardhi za mikoa waendelee kuwa washauri kwa kamati za mipango miji katika mabaraza ya madiwani.

" kama vibali vya ujenzi tuliwaondoa na kupanga pia tuwaondoe, mtafanya kazi gani ? hiyo haiwezekani,  kwa sasa muongozo unaokuja kamati za ardhi na makazi zitapatiwa ufafanuzi wa namna bora ya matumizi ya ardhi na baadaye kupelekwa kwa maafisa mipango miji.