SALVATORY NTANDU,SHINYANGA
Wakazi wa wawili wa Kijiji cha Busongo kata ya Mwamashele Wenslausi James (30) na Betha Kasimili (25), ambao ni wanandoa  wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, wamepoteza maisha kwa kujilipua kwa moto kwa kutumia Mafuta ya Petrol,baada ya wazazi wa upande wa mwanaume kumkataa mwanamke aliyeolewa na kijana wao.

Akizungumza na leo waandishi wa habari kaimu kamanda wa polisi mkoani humo,(ACP) Jackson Mwakagonda amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa wanandoa hao walipoteza Maisha June 14 mwaka huu majira ya saa nne asubuhi.

Amesema kuwa  Wenslaus na Betha enzi za uhai wao wamefanikiwa  kuzaa watoto watatu, lakini wazazi wa upande wa  mwanaume walimkataa mke wa kijana wao na kuamua kuivunja ndoa hiyo na kuamuru mwanamke huyo arudishwe nyumbani kwa wazazi wake Kishapu.

“Baada ya ndoa hiyo kuvunjika Wenslaus, alisikia kuwa mke wake anataka kuolewa, na kuamua kwenda ukweni kwake  akiwa na galoni la mafuta ya Petrol lita tano, na kisha kuingia chumbani kwa Betha na kufunga mlango kuanzisha ugomvi,”alisema Mwakagonda.

Kamanda Mwakagonda   amesema   kuwa Wenslaus  aliamua kumchoma kisu cha ubavuni mke wake, na kisha kumfunga minyororo na kumwagia mafuta ya Petrol kisha na yeye kujimwagia Petrol akawasha kiberiti na kujilipua moto ambao umesababisha wapoteze Maisha.

“Nitoe wito kwa wazazi mkoani hapa, kuacha tabia za kuingilia ndoa za watoto wao, na kuwaonya   wanandoa kutojichukulia  sheria na badala yake wafuate njia za kisheria kutatua migogoro yao ikiwemo,madawati ya jinsia,ustawi wa jamii na viongozi,”alisema Mwakagonda.

MWISHO.