Na Mwandishi wetu- Dodoma

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Brigedia Jenerali  Rajabu Mabele amewataka  vijana wote waliochaguliwa kujiunga na mafunzo ya JKT kwa mujibu wa  Sheria kwa mwaka 2021 ambao hawajaripoti na wale waliochanguliwa kwa awamu ya pili kuhakikisha wanaripoti kwa wakati katika makambi waliyopangiwa kufikia June 17,  2021 ili waweze kuanza mafunzo hayo kwa wakati.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa Tawi la Utawala JKT Kanali Hassan Mabena    Juni 10, 2021, Jijini Dodoma wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu  ya JKT Chamwino mkoani Dodoma.

“Mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria mwaka 2021 yataendeshwa kwa muda wa miezi mitatu tu, vijana hao walioitwa kupitia orodha ya pili na baadhi ya wale  wa awamu ya kwanza ambao hawajaripoti hadi sasa wanatakiwa kuripoti makambi ya JKT  waliyopangiwa mara moja”, alisisitiza  Kanali  Mabena

Akifafanua, Kanali Mabena amesema kuwa kwa wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho (Physical disabilities)  wanatakiwa kuripoti katika kambi ya Ruvu   JKT  iliyopo Mlandizi mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuwahudumia.

Orodha kamili ya nyongeza ya majina ya vijana walioitwa , Makambi ya JKT waliyopangiwa na maeneo yaliyopo pamoja na vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo inapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz.

Aidha, Mkuu wa JKT Brigedia Jenerali   Rajabu Mabele anawakaribisha vijana wote walioitwa ili waweze kujiunga na vijana wenzao katika kujifunza uzalendo, umoja wa kitaifa, stadi za kazi, stadi za maisha na utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa.