Wanaharakati wa upinzani nchini Urusi wamekasirishwa na tuhuma zilizotolewa na rais Vladimir Putin dhidi ya mkosoaji wake aliyeko gerezani Alexei Navalny. 

Putin alitetea kukamatwa kwa Navalny baada ya mkutano wake wa kilele na rais wa Marekani Joe Biden mjini Geneva, kwa kusema alipuuza kwa maksudi matakwa ya kujisalimisha mahakamani mwaka uliopita alipokuwa anapokea matibabu nchini ujerumani baada ya tukio la kupewa sumu. 

Msemaji wa Navalny Kira Yar-mysh ameeleza kushangazwa na tamko hilo huku akituma picha ya kiongozi wake katika ukurasa wake wa twitter akiwa hali mahututi hospitalini nchini Ujerumani. 

Navalny alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Moscow katikati ya mwezi Januari alipokuwa anarejea nyumbani kutoka Ujerumani. Baadae mahakama nchini humo ilimhukumu kifungo cha miaka kadhaa gerezani.