Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet, ametoa wito wa hatua za pamoja kusaidia kushughulikia mporomoko mbaya zaidi wa haki za binadamu duniani, akitaja hali nchini China, Urusi na Ethiopia miongoni mwa mataifa mengine. 

Bachelet ametoa wito huo katika ufunguzi wa kikao cha 47 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi, ambapo amezungumzia hali mbaya ya kiutu jimboni Tigray nchini Ethiopia. 

"Katika jimboni la Tigray la Ethiopia, natatizwa na ripoti za kuendelea kwa ukiukaji wa haki za binadamu, ikiwemo mauaji kinyume cha sheria, ukamataji wa holela, vurugu za kingono dhidi ya watoto na watu wazima. Ripoti za kuaminika zinaonyesha wanajeshi wa Eritrea wanaendelea kutenda ukiukaji wa haki za binadamu na sheria ya kiutu." 

Kikao hicho kitakachodumu hadi Julai 13 na kinachofanyika kwa njia ya mtandao, kinatarajiwa kujadili ripoti inayosubiriwa kwa shauku kuhusu ubaguzi wa kimfumo, na rasimu za maazimio kuhusu hali kadhaa za haki zinazotia wasiwasi, zikiwemo za nchini Myanmar, Belarus na mkoa wa Tigray nchini Ethiopia.