Ripoti ya shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, imesema idadi ya watu wanaoyakimbia makaazi yao kutokana na mizozo, machafuko na ukiukwaji wa haki za binaadamu imeongezeka hadi milioni 82.4. 

Ripoti hiyo mpya iliyochapishwa mjini Geneva Uswisi imesema idadi hiyo imeongezeka mara mbili kwa mwaka uliopita ikilinganishwa na takwimu za muongo mmoja uliopita licha ya janga la virusi vya corona. 

Ripoti hiyo inaonyesha idadi ya watu waliohama ulimwenguni iliongezeka kwa takriban watu milioni 3 mwaka jana, baada ya kushuhudiwa kiwango kilichovunja rekodi mwaka 2019 na kufanya asilimia moja ya watu duniani ama kuondolewa ama kuondoka wenyewe kwenye makaazi yao. 

Raia kwenye mataifa ya Syria, Afghanistan, Somalia na Yemen walilazimika kuondoka huku mizozo nchini Ethiopia na Msumbiji ikitajwa kusababisha watu kuyakimbia makaazi yao.