Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeidhinisha azimio la kisiasa, la kuyamaliza maradhi ya UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Kulingana na azimio hilo wanachama wa baraza hilo kuu wameahidi kupunguza kiwango cha maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI hadi 370,000 na vifo vitokanavyo na UKIMWI hadi chini ya 250,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.
Mkurugenzi Mkuu wa Mpango wa pamoja wa Umoja wa Mataifa kuhusu UKIMWI, UNAIDS, Winnie Byanyima amesema bado mataifa mengi hayajafikia ahadi zao na kuonya janga la COVID-19 linaweza kuibua upya janga la UKIMWI.
Mataifa wanachama yamekubaliana kulimaliza janga hilo kwa kuwafikia asilimia 95 wa watu wanaoishi na VVU, asilimia 95 ya usambazaji wa dawa za kufubaza makali ya VVU na asilimia 95 ya watu wenye virusi sugu dhidi ya dawa.