Watu 34 wamepoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa leo, baada ya treni za mwendo wa kasi kugongana. 

Msemaji wa kampuni ya reli amesema idadi isiyojulikana ya watu walikuwa bado wamekwama kwenye mabaki ya mabehewa karibu na mji wa Daharki, jimbo la Sindh, na kuongeza kuwa waokoaji wameomba haraka kupelekewa vifaa makhsusi kuwasaidia kukata vyuma ili kuwatoa. 

Afisa mwandamizi wa polisi wa mji wa Daharki, Umar Tufail, amethibitisha idadi ya waliopoteza maisha. Picha zilizosambaa kwenye vyombo vya habari zinaonesha miili ikiwa imelazwa chini ikifunikwa sanda nyeupe. 

Waziri Mkuu Imran Khan amesema ameshtushwa na ajali hiyo, na kuahidi uchunguzi kamili. 

Jeshi limetumwa kusaidia juhudi za uokozi. Ajali za treni hutokea mara kwa mara nchini Pakistan, ambayo ilirithi maelfu ya kilomita ya njia za reli kutoka kwa mkoloni wake, Uingereza.