Na Mwandishi wetu, Mtwara
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameelekeza  somo la Elimu kwa Michezo lifundishwe kwa wanafunzi wote katika Shule za Msingi na kuhamasisha wanafunzi wa shule za Sekondari kusoma somo hilo.

Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo Juni 08, 2021 Mkoani Mtwara alipofungua mashindano ya michezo na taaluma kwa shule za msingi na Sekondari (UMITASHUMTA na UMISSETA) ambapo amesema matarajio ya Serikali ni kuona wanafunzi wakionyesha uwezo wao kwa nidhamu ya hali ya juu na kuleta mafanikio kwa taifa.


“Kauli mbiu ya michezo ya mwaka huu inayosema “Michezo, Sanaa na Taaluma kwa Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda” inasadifu kwa kiasi kikubwa nia ya Serikali na Chama Tawala, Chama cha Mapinduzi kutumia kila fursa tuliyo nayo katika kuleta maendeleo ya wananchi wetu na taifa kwa jumla” amesema Mhe. Majaliwa


Ameongeza kuwa  Mheshimiwa Rais ameshatoa maelekezo ya kuiangalia mitaala ya elimu ili  ijielekeze katika kujenga stadi za ujuzi kwa maendeleo ya taifa ikiwemo Elimu kwa Michezo na Sanaa, hivyo kupata wanamichezo na wasanii chipukizi wengi na bora ambao watafundishwa taaluma hizo kuanzia ngazi za awali, msingi, sekondari na vyuo.

Aidha, Serikali inaendela na jitihada za kuanzisha tahasusi zenye la Elimu kwa Michezo kwa wanafunzi wa Kidato cha 5 na 6 ili kupata mafaniko katika sekta yenyewe na kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa viwanda.

“Nasisitiza Wizara husika kuingalia mitaala iliyopo kama inakidhi mahitaji ya sasa na kuchukua hatua stahiki pale ambapo kutaonekana kuna upungufu, nihimize kuboreshwa kwa vyuo vya ualimu  ili viimarishe masomo ya Elimu kwa Michezo hatua itakayomuwezesha kila mhitimu kuwa na ujuzi wa ufundishaji wa michezo.

Pia Mhe. Majaliwa amesisitiza wito wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan wa kuwahimiza wananchi kufanya mazoezi ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukizwa, huku akisisitiza kuendelea kuunda vikundi vya mazoezi ya ukakamavu (Jogging na matamasha mbalimbali ya michezo) na kujijengea utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara kwa afya zenu.


Zaidi ya hayo, Mhe. Majaliwa amewaasa vijana wajiepushe na vitendo vitakavyokwamisha ndoto zao za kufanikiwa katika masomo na michezo kama vile matumizi ya madawa ya kulevya, uvivu na utoro shuleni.  


Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema Wizara hiyo inatarajia kuanzisha kituo maalum cha kuendelezea michezo katika Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya ili kuendeleza vipaji vinavyopatikana. 


Waziri Bashungwa amesema hayo Juni 08, 2021 Mkoani Mtwara wakati wa ufunguzi wa mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi na Sekondari (UMITASHUMTA na UMISSETA).


"Muamko na hamasa unayoiona leo hii, ni ushirikiano wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na  Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia katika ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya mawaziri, makatibu wakuu na wataalam" amesema Waziri Bashungwa. 


Waziri Bashungwa amesema kuwa Wizara yake inashirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kufanya tathimini katika kila mkoa ili kubaini shule zitakazopendekezwa maalum kwa michezo.


"Ni matarajio yetu kwa kuisimamia michezo hii vizuri, itakuwa ni chimbuko kubwa la kuvuna vipaji ambavyo vitaendelezwa, ili kupata wachezaji wenye weledi, watakaochezea timu zetu za Taifa, lakini pia watakaocheza michezo ya kulipwa, na kujipatia ajira" amesema Waziri Bashungwa. 


Katika mashindano hayo, vyama vya Michezo vya Kitaifa, vilabu, watalaam wa kuvumbua vipaji (scouters) kutoka Taasisi ya Mbwana Samata pamoja na watalaam kutoka Sweeden wamealikwa ili kupata furs aya kuvumbua vipaji katika mashindano hayo. 


Naye Naibu Waziri Ofisi Ya Rais TAMISEMI Mhe. David Silinde amesema malengo makuu ya mashindano hayo ni pamoja na kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kukuza vipaji vya michezo kwa kuibua na kujenga umoja wa kitaifa, mshikamano na upendo baina ya wanafunzi wangali katika umri mdogo ili kuimarisha taaluma ya michezo kwa wanafunzi na kuwajengea ujuzi na maarifa


Mhe. David Silinde amesema mashindano hayo yanasaidia kujenga umoja, uzalendo na mshikamano miongoni mwa wanafunzi, walimu na wadau wa michezo nchini pamoja na kujenga ukakamavu na umahiri katika michezo.