Shirika la afya duniani WHO, limewataka wasafiri barani Ulaya kuchukua tahadhari katika kipindi cha mapumziko ya msimu wa kiangazi na kuonya kwamba bara hilo halijaondoka katika kipindi cha hatari katika makabiliano yake dhidi ya Covid-19, licha ya kupungua kwa viwango vya maambukizi katika siku za hivi karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugeni wa WHO kwa Ulaya, Hans Kluge amesema wanatoa tahadhari kutokana hofu ya kuongezeka kwa vitendo vya watu kuongeza mikusanyiko, kufanya safari nyingi kiholela, matamasha makubwa ya muziki na michezo katika siku na majuma yajayo.

Mkurugenzi Kluge, hakupendekeza marufuku ya kusafiri lakini amewataka raia wa Ulaya kufanya safari zao kwa tahadhari kwa zingatio la hali ilivyokuwa mwaka uliopita ambapo kipindi kama hicho cha kiangazi maambukizi yaliongezeka kwa kiwango kikubwa.