Na WAMJW-DOM
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa fedha za kujenga kiwanda cha dawa chenye uwezo wa kuzalisha dawa kwa siku mbili ili kuondoa uhaba wa dawa uliopo na kupunguza bajeti ya dawa zinazonunuliwa kutoka nje ya nchi.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel  wakati akiongea na kituo kimoja cha runinga hapa nchini.

Mhe.Samia Sulluh Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  ameshatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha dawa nchini kitachosaidia kuboresha huduma za afya nchini kwa kuongeza upatikanaji wa hali ya dawa na kupunguza matumizi ya fedha ambazo zingetumika kununua dawa nje ya nchi.

“Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha, sasa kinajengwa kiwanda kule Njombe ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha vidonge maana yake ni kwamba bidhaa za Dawa zitashuka bei, dawa ambayo ilikuwa inanunuliwa mara moja itanunuliwa mara mbili mpaka mara tatu.” Alisema Dkt. Mollel.

Aliendelea kusema kuwa, hali ya huduma za afya inaendelea kuwa bora nchini hususan katika upatikanaji wa dawa, kwani Serikali imeendelea kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya ununuzi wa dawa ili kukabiliana na uhaba uliokuwepo katika kipindi cha nyuma, huku akiweka wazi kuwa, Serikali imeshatoa Bilioni 123 kiasi kilichotoka kabla ya Bajeti ya mwaka huu.

“Kwa kipindi kifupi cha Rais, mama yetu Samia Suluh Hassan alivoingia kwenye Mamlaka, tumepata kiasi cha shilingi Bilion 123 kwaajili ya dawa, hizo ni fedha zilizotoka ndani ya muda mfupi kabla ya hii Bajeti mpya ambayo tumeifanya, ambayo lengo lake ni  kwenda kuimarisha suala la Dawa, Vifaa tiba na Vitendanishi.” Amesema Dkt. Mollel.

Kwa upande mwingine amekiri kuwa, Serikali imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusiana na dawa, huku akiweka wazi kuwa tayari Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima ameshapokea mrejesho kutoka kwa timu ya ukaguzi aliyoichagua kwenda katika hospitali za mikoa na utekelezaji wake unaanza kufanyiwa kazi ili kudhibiti mianya yote ya upotevu wa dawa nchini.

“Ni kweli kumekuwa na malalamiko mengi kuhusiana na suala la dawa, mmesikia Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gajima ameunda timu zimeenda kwenye hospitali zetu zote za mikoa na wameleta mrejesho, sasa suala la upatikanaji wa dawa sio suala tu la fedha, ukiangalia Serikali imekuwa ikitoa mabilioni ya fedha, mwaka uliopita ilitoa Bilioni 270, ikatoa Bilioni 220 tena, kwahiyo tatizo la upatikanaji wa dawa sio la fedha tu bali uwadilifu na uwazi  kwa baadhi ya watoa huduma lakini pia suala la uelewa kwa wananchi.” Alisema

Kwa upande mwingine Dkt. Mollel amesema kuwa, Serikali inaendelea kumalizia mchakato wa Bima ya afya kwa wote, utakaosaidia kila mwananchi kuweza kupata huduma bora katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini jambo litakalosaidia kurahisisha matibabu kwa wananchi.

“Tukienda kuwa na Bima ya Afya kwa wote, maana yake kwenye eneo la afya tunaenda kufanya kila Mtanzania aweze kupata huduma bora za Afya, lakini tunaenda kuondoa tatizo ambalo limekuwa likilalamikiwa siku zote la upatikanaji wa dawa liwe limetatulika.” Alisema.

Hata hivyo, ameweka wazi kuwa, Bajeti yenye weledi mkubwa iliyopitishwa na Bunge ina msaada mkubwa sana katika Sekta ya afya, huku akiweka wazi kuwa bajeti ya Sekta zote kwa kiasi kikubwa zina akisi sekta ya afya, mfano sekta ya maji ni muhimu katika utoaji huduma katika vituo, sekta ya mawasiliano na miundombinu.

“Serikali inapowekeza kwenye sekta nyingine, maana yake ni kwamba Sekta ya afya nayo inaguswa moja kwa moja, mfano Wizara ya Afya inapojipanga kupunguza vifo vya mama na mtoto, wakati mwingine inafika mahali tunagawa simu vijijini ili kuhakikisha uwepo wa mawasiliano ili kumuokoa mama mjamzito.” Alisema.