Rais Joe Biden wa Marekani ameondoka kuelekea Uingereza, kuhudhuria mkutano wa kilele wa kundi la mataifa 7 yenye nguvu kubwa kiuchumi la G7. Hii ni zaiara yake ya kwanza ya nje tangu alipoingia madarakani.
Ziara hiyo ya siku nane inalenga kujenga upya mahusiano kati ya mataifa ya Ulaya na Marekani yaliyozorota katika enzi ya Donald Trump, pamoja na kuyaimarisha upya mahusiano na Urusi.
Ziara hiyo inachukuliwa kama jaribio kuhusiana na uwezo wa rais huyo wa chama cha Democratic katika kukabiliana na kuyakarabati upya mahusiano na washirika muhimu waliochukizwa na vikwazo vya kibiashara vya Trump pamoja na kujiondoa kwenye mikataba ya kimataifa.
Mkutano kati yake na rais wa Urusi Vladimir Putin, Juni 16, mjini Geneva ndio unaochukuliwa kama kilele cha ziara hiyo, na fursa kwa Marekani kuelezea wasiwasi wake moja kwa moja kwa Putin kuhusu mashambulizi ya kimtandao yanayotokea Urusi, uchokozi wa Moscow dhidi ya Ukraine na masuala mengine.