Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametangaza msururu wa masharti mapya ya kupambana na ongezeko la visa vya virusi vya Corona nchini humo. Hatua hizo zilianza kutekelezwa saa kumi jioni (EAT) jana tarehe tarehe 18 Juni.

Kwenye hotuba iliyopeperushwa kupitia runinga Ijumaa usiku, Museveni alitangaza kuwa usafiri wote wa kibinafsi na wa umma nchini umepigwa marufuku kwa siku 42 zijazo isipokuwa kwa huduma muhimu na mizigo.

Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Entebbe na vivuko vingine vya mpaka wa ardhi hata hivyo vitabaki wazi kwa watalii na wale wanaorejea lakini mamlaka zimepewa jukumu la kuhakikisha kuwa hakuna kesi chanya au aina mpya za covid zinazoingia nchini humo .

Amri ya kutotoka nje imesogezwa kutoka saa tatu usiku hadi saa moja usiku na itadumu hadi saa kumi na moja unusu alfajiri .Waendesha pikipiki, wanaojulikana kama Boda Boda wanaruhusiwa kubeba bidhaa tu.

Kazi zote zinazozingatiwa sio za lazima, shule na taasisi za kujifunzia, sehemu za ibada, na hafla za michezo pia zimefungwa kwa siku 42 zijazo.

Vituo vya biashara na maeneo ya biashara pia yamefungwa na wachuuzi wa soko wakiruhusiwa kulala kwenye vibanda vyao.