Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis amekataa takwa la Kadinali wa Kijerumani, Reinhard Marx la kujiuzulu katika kanisa hilo kutokana na kashfa ya unyanyasaji wa kingono inayolikabili, lakini amesema mchakato wa mabadiliko ni wa lazima, na kwamba kila askofu lazima awajibike katika kukabiliana na janga hilo.
Papa alimwandikia barua Askofu Marx, ikiwa ni majibu ya tangazo lake la juma lililopita la kutaka kujiweka kando ya kanisa kama askofu wa Munich, kutokana na namna alivyoshindwa kushughulikia visa vya unyanyasaji wa kingono.
Hata hivyo papa amekataa kukubali hatua ya kujiuzulu kwa askofu huyo badala yake amemtaka aendelee na wadhfa wake wa uaskofu.
Kumekuwa na mabishano makali nchini Ujerumani ambapo wahafidhina katika kanisa Katoliki wamekuwa wakipinga kuanzishwa mjadala wowote wenye kujikita katika masuala kama ya useja, ukuhani, jukumu la mwanamke katika kanisa na ushoga.