Panya wa kiume kutoka Tanzania, Magawa ambaye mwaka jana alitunukiwa nishani ya dhahabu kutokana na uwezo wake wa kubaini mabomu ya kutegwa ardhini Cambodia, anastaafu Mwezi huu.

Magawa alizaliwa Tanzania Nov 5,2014 akiwa na uzani wa KG 1.2 na urefu wa Sentimita 70, alipewa mafunzo na Shirika lisilo la Kiserikali la Apopo kutoka Ubelgiji lenye Makao yake Morogoro Tanzania na alipewa nishani ya dhahabu kutokana na uwezo wake wa kubaini mabomu ya kutegwa ardhini.

Wasimamizi wake wanasema Magawa mwenye umri wa miaka saba kwa sasa ameanza kupunguza kasi yake ya kutegua mabomu kwakuwa amezeeka na ni wakati wake wa kupumzika.

Shirika la Matibabu ya Wanyama la Uingereza lisilokuwa la kiserikali PDSA lilimtunza medali ya dhahabu kwa kujitolea kwake kuokoa maisha kupitia kazi yake ya kubaini mabomu hatari yaliyotegwa ardhini Cambodia, inadhaniwa huenda kuna hadi mabomu Milioni sita ya kutegwa ardhini katika Nchi hiyo ya kusini mashariki mwa bara Asia.