Ndege za kivita za Israel zimeshambulia ukanda wa Gaza, Jumatano asubuhi, baada ya Wapalestina kurusha maputo yenye bomu Kusini mwa nchi hiyo

Jeshi la Israel limethibitisha kushambulia ngome za kundi la Hamas, katika ukanda wa Gaza na kusema liko tayari kwa lolote katika vita dhidi ya kundi hilo.

Aidha, Israel imesema imejibu hatua ya kundi la Hamas, kurusha Maputo hayo yenye bomu ambayo yamesababisha moto kuwaka karibu na mpaka wa Gaza.

Haijafahamika iwapo mashambulizi haya yaliyotekelezwa na jeshi la Israeli yamesababisha maafa au majeruhi katika ukanda wa Gaza, huku msemaji wa Hamas akiliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa, litaendelea na harakati za kutaka kulinda maeneo yao takatifu mjini Jerusalem.

Mashambulizi haya yamerejea kwa mara ya kwanza baada ya usitishwaji wa mashambulizi kati ya Israel na Gaza Mei tarehe 21 kufuatia makabiliano ya siku 11 yaliyosabbaisha vifo vya Wapalestina 256 wakiwemo watoto 66.