Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza Ratiba ya uchaguzi mdogo wa Ubunge wa Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba na Kata 6 za Tanzania Bara.

Tayari Tume imekwisha kupokea Barua kutoka kwa Spika wa Bunge kuwa kiti hicho kiko wazi.

Taarifa iliyotolewa kwa Vyombo vya habari Jijini Dodoma  3 Juni, 2021, na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dk. Willson Mahera imesema uchaguzi huo umeapangwa kufanyika tarehe 18 Julai, 2021.

“Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, ameitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi ya kiti cha Ubunge katika Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba,” alisema Dkt Mahera.

Kiti cha Mbunge wa Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba kiko wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Khatib Said Haji na hivyo kukoma kuwa Mbunge kwa mujibu wa Ibara ya 71(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Aidha, Tume imepokea barua kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa akiitaarifu juu ya kuwepo kwa nafasi wazi za Madiwani kwenye kata sita (06) za Tanzania Bara.