Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa, linamshikilia mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa, Prudence Patrick (22) kwa tuhuma za kumuua kwa kumnyonga shingo mpenzi wake Petronila Mwanisawa (21), mkazi wa Semtema, Kata ya Kihesa, Iringa.

Imedaiwa kuwa mtuhumiwa wa mauaji hayo ni mwenyeji wa Sumbawanga na ni mwanafunzi wa kozi ya uandishi wa habari na marehemu pia alikuwa mwanafunzi mwenzake na alikuwa mwenyeji wa Mkoa wa Kagera.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Juma Bwire, aliwaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake kuwa tukio hilo lilitokea majira ya 12 alfajiri katika eneo la Semtema, Kata ya Kihesa, Manispaa ya Iringa kwenye chumba alichokuwa akiishi mtuhumiwa huyo.

Alisema kuwa mwanafunzi anayedaiwa kunyongwa, alifika nyumbani kwa mtuhumiwa huyo usiku wa kuamkia Juni Mosi mwaka huu akiwa na rafiki yake aliyefahamika kwa jina la Belnada Njafula kwa lengo la kuchukua pesa yake kiasi cha Sh. 5,000 ambayo alikuwa anamdai mpenzi wake huyo.

"Baada ya kufika nyumbani kwa mtuhumiwa rafiki yake aliondoka na kuwaacha wawili hao kwa muda ili walipane deni walilokuwa wakidaiana.

"Hata hivyo, marehemu hakurudi nyumbani kwao hadi pale mwili wake ulipokutwa ndani ya chumba cha mtuhumiwa ukiwa umefungiwa ndani na umelazwa kitandani ukitokwa na povu mdomoni na damu puani," alisema Kamanda Bwire.

Alidai kuwa taarifa za awali za kiuchunguzi zinaonyesha mtuhumiwa baada ya kufanya unyama huo, alitumia simu ya marehemu kutumiana ujumbe na rafiki yake kumjulisha kama ana mimba ya Jay ambaye ni rafiki yake.

"Mtuhumiwa alitumia simu ya marehemu kuchati na rafiki wa marehemu kumjulisha kuwa ana mimba ya Jay na baadaye kuwajulisha wazazi wa marehemu kuwa 'binti yenu amefariki dunia'," alisema.

Kamanda Bwire alisema taarifa za awali kuhusu kifo cha mwanafunzi huyo zilitolewa na wazazi wake kutokana na taarifa walizotumiwa na kijana huyo mtuhumiwa.

Alisema kuwa baada ya kufanya unyama huo, mtuhumiwa alikamatwa na Jeshi la Polisi akijaribu kutoroka kuelekea mkoani Dodoma na alikamatwa maeneo ya Mgongo kilomita chache kutoka maeneo ya Semtema anakodaiwa kufanya mauaji hayo.

Kamanda Bwire alisema mtuhumiwa anashikiliwa na polisi na upelelezi wa tukio hilo unaendelea na pindi utakapokamilika, atafikishwa mahakamani.