Mkuu wa Tume ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa ametowa mwito wa kumalizwa mara moja mifumo ya kibaguzi dhidi ya watu weusi kote duniani kuepusha kilichotokea katika mauaji ya Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika, George Floyd. 

Katika ripoti iliyochochewa na kifo cha Mmarekani huyo aliyeuwawa na polisi wa kizungu, Michelle Bachellet amesema ukandamizaji wa kuwabagua watu wenye asili ya Kiafrika umeondowa utamaduni wa kuvumiliana na badala yake kuchochea ubaguzi kwa misingi ya rangi pamoja na kuzusha machafuko.

Mkuu huyo wa Tume ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa ametangaza mpango wa ajenda nne kwa ajili ya kuleta mageuzi katika suala la kuleta haki na usawa kwenye masuala yanayohusu rangi na kuzitolea mwito serikali kuutekeleza mpango huo. 

Rais huyo wa zamani wa Chile amewasilisha ripoti yake ya kurasa 23 mbele ya Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa ambapo miongoni mwa mapendekezo aliyoyatowa ni kulipwa fidia waliopitia vitendo vya ubaguzi wa rangi pamoja na kuyafadhili makundi ya harakati za kupinga ubaguzi wa rangi kama lile la Black Lives Matter.