Kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi 59 yenye thamani ya shilingi trilioni 2 kuanzia mwezi Aprili hadi Mei mwaka huu. Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Profesa Godius Kahyarara alipokuwa akizindua Baraza la Wafanyakazi wa TIC 4 Juni, 2021 amesema kwamba, usajili wa miradi hiyo umeongeza ajira takribani elfu kumi na mbili (12) nchini.

Katika uzinduzi huo Prof. Kahyarara amewataka wafanyakazi kutekeleza mpango wa kanda maalum za kiuchumi lengo likiwa ni kurahisisha kuwahudumia wawekezaji ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zao.

“Suala la Uwekezaji katika Kanda hizi za kiuchumi matarajio ya serikali ni tofauti na tulivyokuwa tunaona kwani ni muhimu sana kutekeleza maono ya namna hiyo. Ni jambo ambalo hatukutegemea Tanzania kuweza kuvutia wawekezaji na kupatikana kiasi cha shilingi trilioni 2 ndani ya miezi miwili (2) hivyo kwa muktadha huo kwa mwaka mmoja itakuwa trilioni ishirini na nne (24)” amesema Prof. Kahyarara.

Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Dkt. Maduhu Kazi amesema kuwa kumekuwa na ushirikiano wa karibu sana kati ya menejimenti ya TIC pamoja na wafanyakazi hivyo tumeona ufanisi umeongezeka.

Aidha, serikali imeanza kuboresha Uwekezaji kwakuwa imeanza mchakato wa kuwa na benki ya ardhi kwa kuunda timu inayohusisha Wizara ya Ardhi, Wizara ya Uwekezaji, Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na TAMISEMI.