Aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na walinzi wake watano  jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha wakikabiliwa na makosa mbalimbali likiwemo la uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kupokea rushwa.

Sabaya ambaye alisimamishwa na Rais Samia Suluhu Hassan Mei 13, 2021 kupisha uchunguzi alifikishwa mahakamani hapo akiwa amefungwa pingu na baada ya wote kushuka kwenye magari ya polisi, walitakiwa kuchuchumaa na kisha kupelekwa katika chumba maalum na baadaye kuingizwa mahakamani.

Waendesha mashtaka wa Serikali, Tumaini Kweka, Abdallah Chaula na Tresla Garvas mbele ya Hakimu Mfawidhi, Martha Mahumbuga na Hakimu Mkazi Mkuu, Salome Mshasha walisema Sabaya na wenzake walitenda makosa hayo Januari 20 na Februari 9, 2021.

Kweka alisema  Sabaya na wenzake watano anatuhumiwa kwa makosa ya kuunda genge la uhalifu, uhujumu uchumi,  kujipatia fedha kwa njia ya rushwa na utakatishaji fedha ambapo Sabaya alijipatia Sh90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara, Francis Mroso mkazi wa kwa Mromboo ambaye alikuwa anatuhumiwa kwa makosa ya ukwepaji kodi ili amsaidie jambo ambalo ni makosa.

Pia, Sabaya na walinzi wake wawili, Sylivester Nyengu (26) maarufu kicheche na Daniel Mbura (38) wanakabiliwa na  makosa mawili ya ujambazi wa kutumia silaha wakidaiwa kuyatenda Februari 9, 2021.

Wanadaiwa walimfunga pingu na kumpiga Bakari Msangi ambaye ni diwani wa CCM kata ya Sombetin na kumuibia Sh390,000 na pia katika eneo la Bondeni jijini Arusha wakitumia silaha,  Sabaya na walinzi hao wanatuhumiwa kumpiga, kumtishia silaha na kumpora Ramadhani Ayoub simu na Sh35,000.

Kwa kuwa makosa hayo hayana dhamana watuhumiwa hao walipelekwa mahabusu Gereza Kuu la Kisongo  na kesi hiyo kuahirishwa hadi Juni 18, 2021.