Na Eliafile Solla
Kamati ya Taifa ya kugawa ardhi ambayo inaongozwa na Kamishna wa Ardhi Bw. Mathew Nhonge, imekutana na kukaa   Juni Mosi kwa ajili ya kupitia jumla ya maombi 45 ya kumiliki ardhi ambayo yamewasilishwa kwenye kamati hiyo.

Katika kikao hicho, Kamati itapitia ombi moja moja na kujiridhisha kama muombaji ama waombaji wamekidhi vigezo vya kumilikishwa ardhi wanayoomba na kwa matumizi yaliyobainishwa kwa mujibu wa sheria.

Kamati hii inaundwa na wajumbe ambao baadhi yao wametajwa kwa mujibu wa sheria na wengine wanaingia kwenye kamati kutokana na utaalam wao ndani ya sekta ya ardhi.

Wajumbe wa Kamati wanaotajwa kwa mujibu wa sheria ni pamoja na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi na Mipango Miji, Mjumbe kutoka Wizara ya Afya, Maliasili na Utalii, Mifugo, Ulinzi, pamoja na mjumbe kutoka Uwekezaji.

Kamati ya taifa ya kugawa ardhi, inafanya kazi zake kwa mujibu wa Sheria ya ardhi Namba 4 ya Mwaka 1999 pamoja na kanuni zake ambayo imeweka bayana majukumu ya kamati na kwamba mwenyekiti wake ni lazima awe Kamishna wa Ardhi.