Waziri Kassim Majaliwa amesema Serikali ipo mbioni kuanza kutekeleza mradi wa kimkakati wa uzalishaji wa gesi asilia ya kimiminika (LNG) mkoani Lindi utakaogharimu dola za kimarekani bilioni 30.

Amesema kuwa Mradi huo ni moja ya mradi wa kimkakati ambao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amepania kuutekeleza katika awamu ya sita ambao utakapoanza kutekelezwa utatumika kwa kipindi cha zaidi ya miaka 25.

Ametoa kauli hiyo jana  (Jumamosi Juni 5, 2021) wakati wa mkutano na wadau wa maendeleo wa wilaya ya Lindi, katika ukumbi wa hoteli ya Sea View Mjini Lindi.

"Vile viwanja mlivyovichukua anzeni kuvijenga, mradi wa gesi asilia unakuja, nina amini mradi huu ukianza baada ya kukamilisha makubaliano, tutafika hatua nzuri" amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amezitaka Halmashauri nchini ziongeze usimamizi kwenye sekta ambazo wananchi wanazitekeleza kila siku ikiwemo sekta ya kilimo na kuifanya moja ya agenda muhimu kwa kuwa watanzania wengi wanategemea kilimo katika kujipatia kipato.

"Halmashauri zetu nyingi watu wake ni wakulima, wafanyakazi ni asilimia tano tu na hata wafanyabishara ni asilimia ndogo, viongozi simamieni kilimo ili kiimarishe mapato ya mtu mmoja mmoja"

Pia, Waziri Mkuu amewataka wananchi wa Lindi kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuinua uchumi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla "tutumie fursa zilizopo ndani ya mkoa kuhakikisha uchumi wetu unapanda, kila mtu afanye kazi katika eneo lake".

Vilevile, Waziri Mkuu alisema kuwa ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2020/25 inaelekeza kuwa katika kujenga uchumi ni lazima uakisi maisha halisi ya kila siku ya wananchi na uwe uchumi shirikishi na shindani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainabu Telack watahakikisha rasilimali zilizopo mkoani humo zinawanufaisha Wana-Lindi na Taifa kwa ujumla "tumekubaliana kwamba lindi ni tajiri, biashara zote zinazofanyika kwasasa tunakwenda kuzitafsiri katika maisha ya watu wetu".