Samirah Yusuph
Bariadi.
Maafisa uvuvi wilaya ya Busega Mkoa wa Simiyu wametajwa kuwa ni changamoto inayopelekea kukosa mapato ya serikali kuu na kuiomba ofisi ya mkuu wa Wilaya hiyo kuingilia kati  ili wawe na uelewa wa pamoja na kuimarisha makusanyo ya serikali.

Changamoto hiyo imebainishwa na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Simiyu Charles Mkumbwa alipokuwa katika hafla ya uanzishwaji wa ofisi ya TRA wilaya ya Busega ambapo amesema kuwa kumekuwa na changamoto ya kukosa ushirikiano mzuri na ofisi ya uvuvi.

"Tunekuwa tukikosa ushirikiano mzuri na ofisi ya uvuvi ambapo leseni za uvuvi zimekuwa zikitolewa bila ya kibali cha kodi...

Sambamba na hilo tunatarajia kuwa na Ofisi ya forodha ili kudhibiti magendo katika mwambao wa ziwa victoria katika ukanda wa mkoa wa Simiyu ili kudhibiti mapato ya forodha ambayo yanaweza kupotea kwa sababu ya kukosa kituo".

Wilaya ya Busega imekuwa ikifanya vizuri katika makusanyo ya kodi kutokana na uchumi ulio izunguka ambao ni Mbuga ya wanyama ya serengeti na ziwa victoria kabla ya madhara ya mlipuko wa virusi vya korona ilikuwa ikikusanya tsh 350 milioni kwa mwezi na kushika nafasi ya pili ya ukusanyaji wa mapato mkoani Simiyu.

Kufunguliwa kwa ofisi ya TRA wilayani humo inawarahisishia walipa kodi 611 kuepuka kusafiri umbali wa kilometa 130 kufata huduma makao makuu ya mkoa ambapo ilipelekea ugumu kwa baadhi ya walipa kodi hao kulipa kodi kwa hiyari.

Wakizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara katika mji wa Ramadi
Lingo Christina na Kulwa Juma wamesema uwepo wa ofisi hizo katika mji wa Lamadi wenye asilimia 70 ya walipa kodi wote wilaya ya Busega itaongeza mzunguko wa biashara kwa sababu biashara hazitafungwa tena ili kusubiri au kufuata huduma za TRA kwa muda mrefu.

"Itaongeza chachu ya watu kulipa mapato kwa sababu ina kuwa rahisi kupata huduma hivyo wafanya biashara watahamasika kulipa kodi bila kusubiri kufatwa wala kushuritishwa...wingi wa wateja kufuata huduma  mkoani ilipelekea wafanyabiashara kusubiri maafisa wa TRA waanze kufuatalia ndipo walipe kodi kwa sababu ukifika ofisi zao mkoani  inachukua siku nzima  jambo ambalo lililopekea wengi kukwepa kufanya malipo".
 
Akizungumza katika hafla hiyo mkuu wa wilaya ya Busega Tano Mwera amewasisitiza TRA kukutana na wafanya biashara ili kufanya makadilio ya kodi yanayoenda na uhalisia wa biashara ili kuondoa malalamiko kwa wateja wao.

Mwisho.