Waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini Ri Son Gwon amesema nchi hiyo haifikirii kuwasiliana na Marekani.

Katika taarifa iliyochapishwa katika shirika la habari la serikali KCNA Ri amesema Korea Kaskazini haifikirii au hata kuwa na uwezekano wowote wa kufanyika mazungumzo na Marekani.

Kauli ya waziri huyo wa mambo ya nje imetolewa baada ya mjumbe mpya wa Marekani kuhusu Korea Kaskazini kusema mjini Seoul mnamo siku ya Jumatatu, kuwa anatarajia majibu mazuri hivi karibuni juu ya kufanyika mazungumzo na Pyongyang.

Mnamo siku ya Jumanne, dada wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, alisema kupitia taarifa kuwa Marekani imekuwa ikitasfiri kimakosa vitendo vya Korea Kaskazini.

Mpango wa silaha za nyuklia wa Korea Kaskazini umekuwa tatizo gumu kwa Marekani kwa muda mrefu, japo utawala wa Rais Joe Biden ulifanya marekebisho ya sera zake na kusema itatafuta njia nzuri za kuishawishi Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa silaha za nyuklia.