Kiongozi wa Korea Kaskazini amesema nchi hiyo inakaribisha mpango wowote wa kufanyika mazungumzo mapya baina yake na Marekani, lakini kamwe haiweza kuondoa mezani chaguo la vita.

Kim Jong-un amenukuliwa akisema hayo jana Ijumaa na shirika rasmi la habari la nchi hiyo KCNA ambapo amesisitiza kuwa, Korea Kaskazini inapaswa kuwa tayari na kujiandaa kwa makabiliano na Marekani.

Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini amelitaka jeshi la nchi hiyo kujiweka tayari kukabiliana na vitisho vyovyote vya maadui wa nchi hiyo ya Peninsula ya Korea.

Ameashiria ujio wa serikali mpya ya Joe Biden nchini Marekani na kubainisha kuwa, "Pyongyang inapaswa kujiweka tayari barabara hususan kwa makabiliano, kwa shabaha ya kulinda hadhi ya taifa letu."

Ikumbukwe kuwa, Juni mwaka 2019, aliyekuwa Rais wa Marekani, Donald Trump na kiongozi huyo wa Korea Kaskazini walikutana katika mpaka usiokuwa wa kijeshi wa Korea Kaskazini na Korea Kusini.

Kabla ya hapo, wawili hao walikutana mara mbili nchini Singapore na Vietnam, lakini vikao hivyo havijakuwa na tija, kwani Washington iliendelea kuiwekea Pyongyanga vikwazo, huku Pyongyang nayo ikiendelea kufanyia majaribio makombora yake ya balestiki.

Pyongyanga inasema Marekani ilijipotezea fursa hizo za kipekee za kuzika uhasama na kufungua ukurasa mpya wa uhusiano baina ya pande mbili hizo hasimu.

-Parstoday