Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Simon Sirro , ametangaza operesheni ya mwezi mmoja ya kusaka wahalifu nchini.

IGP Sirro ametangaza operesheni hiyo, akizungumza na Makamanda wa Jeshi la Polisi wa Mikoa ya Kanda Maalum ya Dar es Salaam, leo Jumanne, tarehe 8 Juni 2021, jijini humo.

IGP Sirro amesema, operesheni hiyo itaanza kesho Jumatano tarehe 8 Juni 2021.

Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi Tanzania, amewaonya watu wanaopanga kufanya uhalifu, waache mara moja, kwa kuwa jeshi hilo limejipanga kukabiliana nao kwa mujibu wa sheria.

“Kesho tunaanza operesheni ya mwezi mzima na hii operesheni ni ya nchi nzima. Jambo la msingi wale wahalifu waliotoka na kuanza uhalifu mbaya mbaya wasije kulalamika na sie tukiwafanyia mambo mabaya mabaya. Sisi tutafanya mambo mabaya kwa mujibu wa sheria,” amesema IGP Sirro.

Sirro ameongeza “suala la msingi waache uhalifu na kufanya kazi za uhalali, wakienda kinyume wasilaumu jeshi, wasilaumu Serikali.”

IGP Sirro amesema, operesheni hiyo itaenda sambamba na msako wa makosa ya usalama barabarani, ambapo ameagiza Makamanda wa Polisi wa Usalama Barabarani (Traffic) wa Mikoa, kusaka magari mabovu.

“Pia , nimeelekeza operesheni ya usalama barabarani, kuna makosa ya usalama barabarani yameanza kujitokeza kama mnaona, ajali zimetokea ajali. Operesheni dhidi ya magari mabovu itaanza kesho,” amesema IGP Sirro na kuongeza:

“Nawaambia makamanda na wakuu wa Traffic mikoa yote kufanya operesheni, dhidi ya magari mabovu ambayo hayatakiwi kuwa barabarani na wahakikishe wanakua wakali kusimamia sheria za usalama barabarani.”