Idadi ya watu waliouwawa katika kijiji cha Solhan Kaskazini mashariki mwa Burkina Faso imeongezeka na kufikia 160. 

Maafisa wa eneo hilo, wamesema wananchi wameipata miili ya watu 160 wakiwemo watoto 20 kutoka katika makaburi matatu ya pamoja. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea kusikitishwa na mauaji hayo yaliyotokea Jumamosi, katika moja ya mashambulizi mabaya kwenye taifa hilo kwa miaka mingi. 

Guterres amezitaka jumuiya za kimataifa kuongeza kasi katika mapambano dhidi ya wapiganaji walio na itikadi kali. Wahusika na malengo ya washambuliaji, ambao walikilenga kijiji katika jimbo la Yagha bado havijajulikana. 

Makundi kadhaa yaliyojihami kwa silaha yanaendesha shughuli zake katika kanda ya Sahel. Baadhi ya makundi hayo yameonyesha utiifu kwa kundi la Al Qaeda na lile linalojiita Dola la Kiislamu IS.