SERIKALI imekubali hoja za wabunge waliopendekeza kutoza adhabu ya asilimia 100 ya kiwango cha kodi anachokwepa muhusika kupitia biashara katika bidhaa au huduma.

Akijibu hoja wakati wa kuhitimisha majadiliano ya Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2021, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema baada ya kusikia hoja za wabunge serikali imeamua kuchukua ushauri kwa kuweka kifungu kipya cha kubana ukwepaji kodi.

“Makubaliano yaliyofikiwa katika kikao cha leo asubuhi (jana) kati ya serikali na kamati ya bunge ni kufanya mabadiliko kwenye tuliokuwa tumependekeza kuweka asilimia 75 wamependekeza kuwa asilimia 100 ya kodi iliyotakiwa kutozwa”alisema Dk Mwigulu na kuongeza; “Kwa maana hiyo kodi itakuwa imezidishwa mara mbili ya iliyotakiwa kutozwa kama mtu huyo atakuwa amekwepa, kwa hiyo sisi kama serikali tunapokea maoni ya  waheshimiwa wabunge na kamati ambayo ni mwakilishi wa Bunge.”