China imepongeza kuanza tena mazungumzo ya kawaida na Marekani kuhusu biashara na uchumi. 

Naibu waziri mkuu wa China Liu He, ambaye amekuwa akiongoza mazungumzo na Marekani amezungumza mara mbili kwa njia ya video na mjumbe maalumu wa biashara wa Marekani Katherine Tai na waziri wa fedha Janet Yellen katika kipindi cha wiki moja. 

Mazungumzo hayo ni ya kwanza rasmi kati ya nchi hizo mbili kuhusu masuala ya biashara na uchumi chini ya utawala wa rais Joe Biden. 

Msemaji wa wizara ya biashara ya China Gao Feng amewaambia waandishi habari kuwa mazungumzo hayo yameanza vyema na mahusiano ya kibiashara kati ya China na Marekani, hali ya kiuchumi na sera za ndani ni miongoni mwa mada zilizojadiliwa. 

Aidha Gao amesema China na Marekani zimekubaliana kushirikiana kwa masilahi ya pamoja kusuluhisha masuala maalumu kwa wazalishaji na watumiaji bidhaa na kuimarisha mahusiano ya kibiashara na kiuchumi.